Quantcast
Channel: ShaffihDauda
Viewing all articles
Browse latest Browse all 9000

Exclusive: Hali ya Chidiebere ikiwa ni siku 32 baada ya kuvunjika taya

$
0
0
Mke wa Chidiebere aliamua kumchukua mumewake kutoka Shinyanga na kumpeleka Mwanza (kwenye nyumba yao) ili amuuguze kwa ukaribu zaidi
Mke wa Chidiebere aliamua kumchukua mumewake kutoka Shinyanga na kumpeleka Mwanza (kwenye nyumba yao) ili amuuguze kwa ukaribu zaidi

Jumatano October 12 mwaka huu huenda ikawa siku mbaya kupata kutokea kwenye maisha ya mshambuliaji wa Stand United Abasirim Chidiebere, huenda ikawa ni siku ambayo hatoisahau katika maisha yake kutokana na ajali ya kisoka aliyoipata siku hiyo.

Siku hiyo Chidiebere alivunjika taya wakati akiitumikia timu yake kwenye uwanja wa nyumbani (CCM Kambarage, Shinyanga) wakati ikichuana na Azam FC na Stand wakafanikiwa kushinda kwa goli 1-0 ukiwa ni ushindi pekee kwa kocha Athuman Bilal tangu alipokabidhiwa timu kutoka kwa Patrick Liewig.

Ni mwezi mmoja sasa umepita tangu Chidiebere aumizwe vibaya na mlinzi wa kati wa Azam FC Agrey Morris tukio ambalo liliwastusha watu wengi.

Akiwa hospitali akipatiwa matibabu mara baada ya kuvunjika taya wakati wa mchezo wa Stand United dhidi ya Azam FC
Akiwa hospitali Shinyanga mjini akipatiwa matibabu mara baada ya kuvunjika taya wakati wa mchezo wa Stand United dhidi ya Azam FC October 12

shaffihdauda.co.tz ilipiga hodi nyumbani kwa Chidiebere maeneo ya Igoma-Mwisho jijini Mwanza ambako mshambuliaji huyo anaishi na mkewake pamoja na mtoto wao Chinonso Chidiebere ili kumjulia hali nyota huyo aliyepata kuichezea Coastal Union katika msimu uliopita kabla ya kushuka daraja.

Hali ya Chidiebere kwa sasa

Hadi sasa Chidi anaenedelea vizuri ukilinganisha na hali yake ilivyokuwa mwanzo. Mwanzo sura yake ilikuwa imevimba sana, lakini kwasasa jamaa yuko poa ana sura ya furaha na bashasha na ukimuona unagundua yuko poa.

Bado hawezi kuongea kutokana na waya maalum alizofungwa ambazo zinamsaidia kushikilia taya ili zipone kwa haraka. Hivyo mawasiliano na Chid yalikuwa ni kwa njia ya ujumbe mfupi wa maandishi (SMS) au unaweza kumuuliza kitu kawaida kwasababu anasikia vizuri lakini yeye anakujibu kwa SMS.

Chidiebere hawezi kabisa kufungua kinywa chake kutokana na kufungwa waya maalum zinazoshikilia taya zake
Chidiebere hawezi kabisa kufungua kinywa chake kutokana na waya maalum alizofungwa zinazoshikilia taya zake

Alielezea hali yake kwa sasa kuwa inazidi kuimarika na anamatumaini makubwa ya kurejea tena uwanjani baada ya kupona lakini mwanzo alikata tama kama ataweza kurudi uwanjani na kucheza kama zamani kutokana na maumivu makali ya kichwa aliyokuwa akiyapata wakati huo. Anasema wakati mwingine alikuwa anahisi maumivu makali kwenye masikio.

“Mara ya kwanza hali ilikuwa mbaya, nilipoteza matumaini kama ntarejea tena uwanjani, lakini kwasasa mambo yanaenda poa hali yangu inazidi kuimarika siku hadi siku. Mungu akipenda ntarudi uwanjani kupambana kwa ajili ya timu yangu (Stand United).”

Mke wa Chidi

Mwanadada Thabitha James ndio mama watoto wa mshambuliaji huyu mkakamavu na mwenye misuli iliyojengeka kwa mazoezi. Nazungumza nae ili kujua kwa undani mambo kadhaa kuhusu maisha ya baba watoto wake baada ya kupata majeraha makubwa.

Alipokeaje taarifa za mumewe kuumia vibaya?

Mama Chinonso anasema, siku hiyo hakufatilia kabisa mchezo wa Stand United vs Azam licha kuwa ni kawaida yake kufatilia kila mechi ambayo inahusisha timu ya mwandani wake. Lakini alistushwa na simu kutoka kwa viongozi wa Stand United wakimpa taarifa za muwake kuumia, mwanzo alipata mshtuko na kudhani huenda Chid amefariki kutokana na namna alivyofikishiwa taarifa.

Chidiebere amebakiza wiki moja na siku mbili ili atolewe waya alizofungwa kwa ajili ya kushikilia taya zake. Waya hizo aliambiwa atakaanazo kwa muda wa wiki 6 sawa na mwezi mmoja na wiki 2
Chidiebere amebakiza wiki moja na siku mbili ili atolewe waya alizofungwa kwa ajili ya kushikilia taya zake. Waya hizo aliambiwa atakaanazo kwa muda wa wiki 6 sawa na mwezi mmoja na wiki 2

“Siku hiyo sikuangalia mechi kwasababu hapa jirani kulikuwa na harusi, nikapokea simu kutoka kwa viongozi wa timu lakini walikuwa wanadhani niliangalia ile mechi. Nilipokea simu nikaambiwa ‘Chid mzima usisikilize maneno ya vyombo vya habari’ nikashtuka sana kwasababu sikuangalia mechi na sikuwa najua chochote kinachoendelea.”

“Kwa kawaida Chid anapoingia uwanjani huwa ananiambia na akitoka ananiambia wameshamaliza mechi, lakini siku hiyo sikupata taarifa yoyote baada ya mechi kumalizika, hicho kitu kikazidi kunipa wasiwasi.”

“Nikaomba aliyenipa taarifa anipe fursa ya kuongea na Chid, akaniambia haiwezekani kwasababu yupo hospitali, hapo nikazidi kuchanganyikiwa nikajua Chid hatunae tena. Nikazidi kuomba wanipe nafasi japo ya kuongea nae, kiongozi akaniambia wewe jua tu Chid ameumia taya zote zimevunjika, nilipata shida sana.”

Ilikuaje ulipokunata na Chid kwa mara ya kwanza baada ya kuumia

Mke wa Chid hakuweza kuonana na Chid siku ambayo aliumia kwasababu yeye anaishi Mwanza wakati Chid anaishi kazini kwake Shinyanga, ikabidi alale halafu kesho yake ndio asafiri hadi Shinyanga kumuona tulizo la moyo wake.

“Usiku ulikua mrefu sana, sikulala vizuri kutokana na mawazo niliyokuwa nayo juu yake, kuna wakati nilikuwa nahisi nadanganywa tu ila Chid sio mzima tena.”

Chidiebere ni baba wa mtoto mmoja anayeitwa  Chinonso Chidiebere amabye pia ameonesha kufata nyayo za baba yake kutokana na kupenda kucheza mpira
Chidiebere ni baba wa mtoto mmoja anayeitwa Chinonso (Mungu pamoja nasi) amabye pia ameonesha kufata nyayo za baba yake kutokana na kupenda kucheza mpira

“Kesho yake nikaenda hadi hospitali nikaonana nae, kibaya zaidi alikuwa haongei kwahiyo tukawa tunawasiliana kwa njia ya SMS tu.”

“Sikutaka kumuonesha maumivu niliyokuwanayo ndani yangu kwasababu nilihisi nitamuumiza zaidi, kwahiyo muda mwingi nikawa namtania sana na kumfanya atabasam huku nikimtia moyo kwamba atapona. Nashukuru hata viongozi na wachezaji wanzake pia hawakuonesha huzuni zao mbele yake tukawa tunamtania na kucheka, alifarijika sana na kuona ni jambo la kawaidia tu.”

Mke wa Chid anaamua kumchukua mumewake na kumrudisha Mwanza

Inawezekana wengi wakajiuliza kwanini Chid aliondoka Shinyanga na kwenda Mwanza badala ya kubaki chini ya uangalizi wa daktari wa timu huku akipatiwa huduma kwa gharama za timu na kujua maendeleo yake ya kila siku.

Mke wa Chid aliamua kumchukua mumewe kwa ruhusa maalum kutoka kwa uongozi wa Stand United chini ya daktari wa timu.

Chidiebere, kewake na rafikiake wakiwa jukwaani wakishuhudia mechi ya Stand United vs Simba. Chid alihudhuria mechi hiyo baada ya kutoka hospitali kuangalia maendeleo ya afya yake
Chidiebere, mkewake na rafikiake wakiwa jukwaani wakishuhudia mechi ya Stand United vs Simba. Chid alihudhuria mechi hiyo baada ya kutoka hospitali kuangalia maendeleo ya afya yake

“Mimi ni mkewe, niliamua kumchukua ili kumhudumia kwa karibu zaidi, naweza kumhudumia na kumsaidia kwa ukaribu zaidi kuliko mtu mwingine. Viongozi waliniuliza ni wapi nitakuwa huru zaidi kukaa na mgonjwa, nikawaambia ni bora nirudi nae nyumbani, wakaniruhusu na daktari akanipa maelekezo yake kuhusu vitu vya kuzingatia.”

Vipi kuhusu support kutoka Stand United?

Mke wa Chid amekiri kuwa, uongozi wa Stand United upo karibu nae na wanasaidiana kwa pamoja kuhakikisha Chid anapona na kurejea kwenye hali yake ya kawaida.

“Kiukweli wananisaidia, kwasababu tangu mwanzo wakati nawaomba niondoke na Chid nirudi nae nyumbanni wako pamoja na mimi.”

Changamoto za kumuuguza Chid

Kama unavyojua Chid hawezi kabisa kufungua kinywa chake hata kidogo. Kwahiyo anakula vyakula laini (vya majimaji) kwa mrija kupitia sehemu ambapo lilitolewa jino moja ili kuwezesha mrija huo kupita na kumfanya aweze kula. Kwahiyo changamoto kubwa iliyotajwa na mkewe ni kuandaa chakula cha jamaa.

Kuandaa chakula cha mgonjwa ndio changamoto kubwa anayoipata kila siku mke wa Chidiebere
Kuandaa chakula cha mgonjwa ndio changamoto kubwa anayoipata kila siku mke wa Chidiebere

“Chid ni mchezaji na ni mtu wa mazoezi kwahiyo inabidi apate chakula chenye virutubisho vingi ikiwa ni pamoja na nilivyoelekezwa na daktari.”

“Namtengenezea uji wa lishe, juice, mbogamboga, ndizi, viazi na hivyo vyote inabidi visagwe. Changamoto kubwa ninayoipata kwa sasa ni kusaga chakula chake, natumia mkono kwasababu umeme bado haujafika mtaani kwetu kwahiyo nyumba yetu haina umeme hivyo siwezi kutumia blender.”

Chid anakula kinoma

“Kila anavyozidi kupata nafuu kilo za chakula zinaongezeka, mwanzoni alikuwa hawezi kula sana kwasababu sehemu aliyokuwa anapitishia chakula ilikuwa bado inamuuma kwasababu ya kidonda kilichotokana na kung’olewa jino lakini kwa sasa yuko vizuri anakula zaidi ya kilo tatu kwa siku.”

Usimchukulie poa Chid linapokuja suala la msosi, jamaa licha ya kula kwa kutumia mrija, anaondoka na zaidi ya kilo 3 kwa siku
Usimchukulie poa Chid linapokuja suala la msosi, jamaa licha ya kula kwa kutumia mrija, anaondoka na zaidi ya kilo 3 kwa siku

“Kwahiyo inanilazimu kutumia muda mwingi kuandaa chakula chake ambacho nakisaga na kukichuja kwa kutumia chujio la chai ili kiweze kupita kwenye mrija.”

Kitu ambacho anamisi mke wa Chid kutoka kwa muwake baada ya kuumia

“Sasahivi na-miss kumsikia Chid kwasababu tumezoea kutaniana sana, tunaishi kama mtu na mtani wake lakini sasahivi kama nikitaka kuwasiliana nae namwambia kwa mdomo yeye ananijibu kwa SMS au kwa ishara na yeye akitaka kuniambia kitu ananiandikia SMS halafu mimi namjibu kwa kawaida tu.”

Licha ya kipato kidogo anachopata kutokana na kazi yake ya soka, Chidiebere amejenga nyumba Igoma jijini Mwanza ambapo anaishi na mkewe pamoja na mtoto wao
Licha ya kipato kidogo anachopata kutokana na kazi yake ya soka, Chidiebere amefanikiwa kujenga nyumba Igoma jijini Mwanza ambapo anaishi na mkewe pamoja na mtoto wao

www.shaffihdauda.co.tz na wadau wote wapenda soka, wanamuombea na kumtakia kila laheri Chidiebere Abasarim apone haraka na kurejea tena uwanjani kuisaidia timu yake ya Stand United.


Viewing all articles
Browse latest Browse all 9000

Trending Articles



<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>