Na Baraka Mbolembole
GOLIKIPA mzoefu na nahodha wa zamani wa Taifa Stars, Juma Kaseja amesajiliwa katika timu ya Kagera Sugar FC.
Lakini kocha Mexime Mexime hajaishia hapo ameongeza nguvu zaidi katika kikosi chake kilicho nafasi ya nne katika msimamo kwa kuwasaini mlinzi wa kati, Mohamed Fakhi aliyeshindwa kuelewana na uongozi wa African Lyon.
Wawili hao wanataraji kuimarisha safu ya ulinzi ya timu hiyo ya Bukoba iliyoruhusu magoli 16 katika michezo 15 ya mzunguko wa kwanza.
Kagera ambayo inamtegemea zaidi kijana Mbaraka Yusuph katika ufungaji imemsaini pia mshambulizi wa zamani wa Mtibwa Sugar, Ame Ally ‘Zungu’ ambaye alishindwa kutulia katika kikosi cha Azam FC msimu uliopita na kupelekwa Simba SC kwa mkopo msimu huu.
Ame alikuwa chaguo la nne katika safu ya mashambulizi katika timu ya Simba lakini anaweza kufanya vizuri katika timu yake mpya kutokana na mahusiano yake mazuri kikazi na Mexime ambaye walifanya kazi pamoja katika kikosi cha Mtibwa Sugar msimu wa 2014/15.
Kagera imefanikiwa kufunga magoli 16 katika michezo ya mzunguko wa kwanza na usajili huu wa Ame unatarajiwa kuongeza makali katika safu ya mashambulizi ambayo ilisuasua sana katika michezo ya mwanzoni mwa msimu.