Na Abubakar Khatib “Kisandu”, Zanzibar
Kiungo mshambuliaji wa Taifa Jangombe Abdallah Mundhihir ‘Mido’ huenda akajiunga na timu ya Stand United ya Shinyanga ya ligi kuu soka Tanzania bara.
Baada ya kuzagaa taarifa hizo Mtandao huu umeamua kumtafuta mchezaji huyo ambapo yeye mwenyewe amethibitisha kuwa kweli Stand wanamuhitaji na kesho (Alhamisi, December 15) anakwenda Dar kumalizana nao ambapo kesho ndio mwisho wa dirisha dogo la usajili ligi ya bara.
“Hizo habari kweli zinazungumza lakini kuweka wazi sasaivi bado mapema, ila kweli Stand nimewasiliana nao, na kesho natarajia kwenda Dar, lakini kwasasa bado mapema kesho tutajua kama ntajiunga na Stand naomba waniombee dua mashabiki wangu wanaopenda maendeleo yetu ya Zanzibar,” anasema Mido.
Abdallah amecheza takribani mechi 7 za ligi kuu soka ya Zanzibar na amefanikiwa kufunga jumla ya mabao 4 katika ligi hiyo ambapo amekuwa muhimili mkubwa wa Taifa ya Jangombe tangu ilipokuwa daraja la Pili.