Kocha Louis Van Gaal amemtaja mlinzi wa kati wa timu yake Chris Smalling kuwa anaweza kuja kuwa nahodha siku moja baada ya Rooney na Carrick kutoweka.
Van Gaal ameyasema hayo zikiwa zimesalia siku kadhaa tu kuelekea mchezo wa ‘Manchester Derby’ kati ya Manchester United na Manchester City Jumapili hii, huku Smalling akiwa ndiye mchezaji bora wa klabu tangu kuanza kwa msimu huu.
Ratiba kama hii msimu uliopita ilikua ni mbaya kwa beki huyo baada ya kutolewa nje kwa kadi nyekundu kabla ya mapumziko dhidi ya City raundi ya kwanza ya ligi.
Smalling ambaye sasa amezaliwa upya, anaelezewa na Van Gaal kama mchezaji anayeshika maagizo yake haraka. “Uwezo wake wa kujiamini na kuongea ndio siri ya yeye kufanya vizuri” anasema Van Gaal alipoulizwa amemsaidiaje Smalling abadilike haraka ndani ya miezi 12.
Van Gaal anasema, “Rooney ndiye nahodha, na Carrick pia, lakini watakapoondoka, bila shaka Smalling ana sifa zote za kuwa kiongozi hapa”.
Uwezo wa Smalling msimu huu haujateka hisia za Manchester United pekee bali timu ya taifa ya England ambapo sasa kocha Roy Hodgson anamtazama mlinzi huyo kama sehemu muhimu ya timu.