
Katika soka la Tanzania vilabu vya Simba na Yanga ndiyo vilabu vikongwe hapa nchini vikiwa na mashabiki lukuki kila kona ya nchi. Vilabu hivyo vimekuwa na burudani nyingi sana lakini siku za hivi karibuni wasemaji (maafisa habari) wa vilabu hivyo wamegeuka na wao kuwa burudani kutokana na tambo pamoja na ‘madongo’, vijembe na sinema wanazozicheza katika kutekeleza majukumu yao.
Siku moja baada ya msemaji wa Simba Haji Manara kulalamikia mabadiliko ya kanuni yaliyofanywa na shirikisho la soka Tanzania (TFF) za kuwatumia moja kwa moja wachezaji waliokamilisha usajili wao kwa njia ya mtandao akidai mabadiliko hayo yamelenga kuipendelea klabu ya Yanga kwani Simba ilishindwa kuwatumia wachezaji iliyokamilisha usajili wao kwa katazo la TFF wakitakiwa kusubiri hadi kamati ya sheria na hadhi za wachezaji ihakiki usajili wao.
Afisa habari wa Yanga Jerry Muro amejibu mapigo hayo ya Manara kwa kukumbusha sakata la mchezaji wa Simba kufaidika na kanuni ya kuchagua mchezo wa kukosa wakati mchezaji huyo alikuwa akitumikia kadi tatu za njano.
Lakini Muro alikwenda mbali zaidi na kuanza kuhoji elimu ya Manara lakini hakuishia hapo akaanza kutamba pia juu ya maisha yake binafsi pamoja na elimu yake.
Hii hapa video ya Muro akitamba dhidi ya Haji Manara wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari December 18, 2015.