Na Baraka Mbolembole
NAAMINI John Bocco ni mfungaji hatari zaidi ya Doland Ngoma, lakini ni kwa nini ‘mfalme’ huyu wa klabu moja anaondolewa katika ‘himaya’ yake? Umeamini Azam FC ni ‘figa la Tatu’ katika soka la Tanzania baada ya Yanga na Simba? Upande wangu niliamini hivyo mara tu baada ya Saad Kawemba kupewa nafasi ya utendaji mkuu wa klabu hiyo iliyoanzishwa mwaka 2007.
Sikuwahi kuamini Azam FC ni ‘washindani wenye mabadiliko’ kwa sababu ‘palipo na pesa ndipo pajaapo watu.’ ‘Majungu’ ni sehemu ya maisha ya mwanadamu, chuki ni visasi visivyo na mwisho na ndani ya klabu hiyo ‘Majungu ndiyo Mtaji.’
Achana na namna walivyoondolewa ‘wapambanaji’ kama Habib Kondo, Mohamed Seif ‘King’-makocha ambao walitengeneza historia ya kuipandisha ligi kuu Azam FC mwaka 2008, lakini walikuja kupuuzwa na kudharauliwa mara tu ya klabu kubadilika ghafla ‘kutoka klabu ya kawaida hadi kuwa klabu tajiri’ katika soka la Tanzania na pengine Afrika Mashariki yote.
Matatizo yalianza kitambo
Miaka kadhaa iliyopita niliwahi kuandika makala nikimshauri mmiliki wa Azam FC kuachana na watendaji wa ndani na kujaribu kuwaajiri raia wa kigeni katika idara nyeti za kiuongozi klabuni hapo. Naamini mmiliki wa klabu hiyo anahitaji kuona timu yake ikipiga hatua ndani na nje ya uwanja na baada ya kuona mambo hayaendi vile anavyotaraji chini ya watendaji wazawa.
Mmiliki naamini ana uwezo wa kuajiri watendaji wa kimataifa ambao wanaweza kumtengenezea ‘mwanga’ wa kule klabu itakapokuwa baada ya muda fulani. Kuendelea kuwaajiri wazawa ni tatizo ambalo leo hii linaifanya Azam FC kupita katika matarajio niliyowahi kuyasema miaka kadhaa iliyopita-klabu kukosa ‘dira’ ambayo ingetuonesha muelekeo wa klabu hata kama timu isingekuwa ikishinda mataji.
Taji la VPL 2013/14 na lile la klabu bingwa Afrika Mashariki na Kati-Kagame Cup 2015 ni mafanikio kwa klabu iliyo na miaka kumi tu tangu kuanzishwa kwake lakini bado nilisema Azam FC si ‘changamoto mpya’ katika soka la Tanzania kwa sababu hadi sasa sifahamu Azam FC inakwenda katika mwelekeo gani.
Mtibwa Sugar FC ilipanda ligi kuu mwaka 1997 na kufikia mwaka 2000 walikuwa na mataji mawili ya ligi kuu na ikumbukwe wakati huo mpira ulikuwa ukichezwa kwa kiwango cha juu na timu yenye ubora ilikuwa na nafasi ya kushinda ubingwa si kama ilivyo sasa-timu yenye pesa zaidi ndiyo hushinda taji.
Azam FC inaelekea walipo Mtibwa Sugar na wanaoipeleka shimoni klabu hiyo ni wamiliki wenyewe kwa kuwaajiri watu ‘wabinafsi’ wenye ‘mapenzi na klabu za Simba na Yanga.’ Kwa nini wasiwaajiri watendaji wa kimataifa katika idara ya utendaji?
Wanajidanganya sana na kudanganywa kuhusu ‘wapiga majungu’ na wanaotaka kuonekana ‘miungu-watu.’ Hawa ndiyo waliwaondoa kina King na Kondo bila thamani, ni hawa waliwaondoa rundo la wachezaji bora na kuwasaini ‘magarasa wa kimataifa’ kwa gharama ya juu.
Wakati wanawaondoa kina King na kuwaajiri Wabrazil mwaka 2009 walisema watengeneza ‘utambulisho wao’.
Walipokuwa wakiwaondoa kina Boniface Pawasa, Shaaban Kisiga, Shekhan Rashid na kuwasaini Wakenya Ibrahim Shikanda, Osborn Monday, Francis Ouma na Mganda, Peter Shenyonjo naamini ilikuwa ni sehemu ya kuimarisha timu kinidhamu, kiubora, na kiufundi hasa ukizingatia vijana kama Himid Mao, Bocco, Salum Abubakary, Salum Machaku wakipandishwa katika timu.
Wapo walioamini Azam FC itafanikiwa haraka na kusahau watendaji wao walikuwa-ama wanachama wa Simba au Yanga.
Kuondolewa kwa Bocco
Nilimsikia msemaji wa klabu ya Azam FC akielezea kuachana na Bocco aliyemaliza mkataba wake. Wakati akizungumza nilikuwa makini kusikiliza sababu hasa ya kuondolewa kwa mfungaji huyo wa muda wote wa klabu na baadae nikagundua hakukuwa na sababu yoyote ile ya maana pale aliposema, “Tumeshamtaarifu mwalimu kuwa hatutokuwa na Bocco msimu ujao.”
Kwa maneno ya Jafar Idd ni kwamba Bocco ameachwa na uongozi si kocha ndiyo maana uongozi umemtaarifu kocha kuachana na Bocco na si kocha kuwataarifu viongozi. Hivi ndivyo sajili za watu wa Simba au Yanga hufanyika na sasa Azam FC imeshika hatamu katika hilo.
Kuondolewa kwa Bocco ni muendelezo tu wa viongozi wa klabu hiyo kuwaacha wachezaji bora. Jabir Aziz, Malika Ndeule, Kipre na ndugu yake wote waliondolewa huku mchango wao ukiwa bado unahitajika klabuni hapo lakini kwa sababu zisizo za kimpira wachezaji hao wakaachwa waondoke.
Naamini mchezaji kama Bocco alistahili kuendelea kuthaminiwa ndani ya Azam FC na namtazama kama mchezaji wa klabu moja tu kama ilivyo kwa nyota wa kimataifa kama Francesco Totti ‘King of Rome’, Ryan Giggs, Phillip Lamh na wengineo ambao walizitumikia klabu moja kwa maisha yao yote ya soka.
Bocco akiwa na umri wa miaka 27 tu ameondolewa Azam FC kwa sababu kuna baadhi ya watendaji hawakutaka kuona mchezaji huyo akiendelea kuboresha rekodi zake. Unaachaje kumsaini Bocco na kuwasaini wachezaji ‘magarasa’ kutoka nje kwa zaidi ya dola 60, 000?
Nasikia kuna viongozi walitaka ‘kupiga 10%’ lakini Bocco akakataa matakwa yao, tatizo likaanzia hapo na kwa vile wao ndio wameshikilia ‘mpini’ wakaamua walichoamua. Kumuondoa Bocco ni sehemu tu ya ‘hujuma’ ambazo watendaji wa klabu hiyo wamekuwa wakizifanya lakini wanasahau kuwa kufanya hivyo ni kuendelea kuiumiza klabu.
Miezi 10 iliyopita
Niliandika makala, ‘Waambieni Wahispaniola wa Azam FC, Bocco hagusiki Azam FC…’ niliandika kwa sababu sikuona sababu ya kuachwa kwake ambazo zilitolewa na kocha Zeben Hernandez na kwa jinsi wawili hao walivyofanya kazi kwa miezi 6 ni wazi tamko lile halikuwa limetolewa na kocha yule raia wa Hispania zaidi lilitolewa na uongozi wake wa juu.
Hii ndiyo sehemu ya makala hiyo…
Una akili kweli wewe, utoke kwenu afu uje utuambie ‘Mr. AzamFC’ hana hadhi ya kuichezea Azam!! Pumbavu zenu. Ujio wenu tu mimi niliuchukia, na mnaanza kunipa sababu za kuwachukia zaidi… Waambie kuhusu Bocco, Himid na Sure Boy. Kwanza, waambie kuwa Bocco ndiye aliyeipandisha ligi kuu timu ya Azam FC mwaka 2008. Ni shujaa wa kukumbukwa wa timu.
Pili, waambie kuwa Bocco huyuhuyu ndiye mfungaji bora wa Ligi kuu Tanzania Bara wakati Azam FC ilipomaliza ‘TOP 2’ kwa mara ya kwanza msimu wa 2011/12. Ni shujaa wa timu. Tatu, Waambie kuwa Bocco ndiye mchezaji aliyefunga goli la ubingwa wakati Azam FC iliposhinda taji lake la kwanza na la pekee katika VPL msimu wa 2013/14. Hagusiki.
Waambie kuwa ‘hirizi’ yenu hiyo ya bahati ndiye mchezaji aliyeipa Azam FC taji la kwanza la kimataifa (Kagame Cup 2015.) Zaidi waambieni ukweli tu kuwa Azam FC inaweza kucheza bila Bocco uwanjani lakini si kumuondoa katika timu. Hagusiki!
Mwisho wa kunukuu makala yale…