Kiungo wa Singida United Mudathir Yahya amecheza kwa kiwango cha juu kwenye mchezo wa kirafiki kati ya Taifa Stars dhidi ya Benin uliomalizika kwa sare ya 1-1 huko nchini Benin.
Mudathir hakuitwa kwa muda mrefu kwenye kikosi cha Stars, mara ya mwisho kuitumikia timu ya Taifa ilikuwa November 2015 ambapo Stars ilifungwa 7-0 ugenini na Algeria kwenye mechi za awali kuwania kufuzu michuano ya kombe la Dunia hiyo ni baada ya kutoka sare ya 2-2 kwenye mechi ya kwanza iliyochezwa uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Katika mechi hiyo (Algeria 7-0 Tanzania) Mudathir Yahya hakumaliza dakika 90 kufuatia kuoneshwa kadi nyekundu na mwamuzi
Imepita takribani miaka miwili tangu Mudathir alipocheza mechi ya mwisho kabla ya mchezo wa leo, kiwango chake katika mchezo wa leo dhidi ya Benin kilikuwa ni cha juu kutokana na kutimiza majukumu yake kwa asilimia nyingi.
Kwa sasa Mudathir anacheza kwa mkopo katika kikosi cha Singida United akitokea Azam, amekuwa na mchango mkubwa kwenye klabu yake huku akivaa kitambaa cha unahodha kutokana na nahodha mkuu wa timu hiyo (Nizar Khalfani) kukaa benchi kwenye mechi nyingi tangu kuanza kwa msimu huu.
Mudathir Yahya pamoja na Jonas Mkude walirejeshwa kwenye kikosi cha Stars kuziba nafasi ya kiungo Mzamiru Yassin na ‘kiraka’ Erasto Nyoni ambao kwa pamoja wanatumikia kadi nyekundu walizooneshwa kwenye mchezo wa kirafiki kati ya Tanzania dhidi ya Malawi uliochezwa uwanja wa Uhuru.
Kwa upande wangu, Mudathir ndio mchezaji bora wa mchezo (man of the match) kati ya Benin dhidi ya Tanzania.
- Katika mchezo wa leo, Benin ndio walikuwa wa kwanza kupata bao kwa mkwaju wa penati bao likifungwa na nyota wa nchi hiyo Stephano Sessegnon dakika ya 30.
- Elias Maguli akaisawazishia Stars dakika ya 50 kipindi cha pili akiunganisha krosi ya Shiza Kichuya.
- Ni sare ya pili mfululizo kwa Stars baada ya kupata sare kama hiyo (Tanzania 1-1 Malawi) ikiwa ni mechi ya kwanza ya kirafiki ya kalenda ya FIFA Stars kucheza ugenini (tangu timu iwe chini ya Salum Mayanga) baada ya kucheza nyumbani mechi zake zilizopita.