Manchester City itaumana na mabingwa wa Ufaransa Paris St-Germain kwenye robo fainali yao ya kwanza ya michuano ya vilabu bingwa Ulaya.
City ni klabu pekee kutoka England iliyobaki kwenye michuano hiyo imebahatika kuzikwepa Bayern Munich chini ya kocha wao mpya wa msimu ujao Pep Guardiola pamoja na mabingwa watetezi Barcelona ambao walikuwa kikwazo kwao kwenye misimu miwili iliyopita ambapo Man City walitupwa nje ya michuano hiyo na vilabu hivyo viwili.
Barca wao wanakutana na wapinzani wao wa kwenye ligi ya Hispania (La Liga) Atletico Madrid wakati Bayern Munich watachuana na Benfica huku Real Madrid ikipambana na Wolfsburg.
Mechi za hatua ya robo fainali zitaanza kuchezwa April 5-6 na 12-13 kuanza kuzisaka timu nne zitakazofuzu kwa ajili ya nusu fainali msimu huu.
Ratiba kamili ipo kama ifuatavyo:
Wolfsburg v Real Madrid
Bayern Munich v Benfica
Barcelona v Atletico Madrid
Paris St-Germain v Manchester City