Naamini kiafya mpo safi na kwa sasa mnaendelea vyema na shughuli zenu za hapa na pale. Mimi pia ni mzma kwani kadi nyekundu 3 za Arsenal ndani ya mechi 2 nimeziona vizuri. Kiwango kizuri cha Cesc Fabregas na mbio za Walcott niliziona pia baada ya kuwa mzma wa afya. Hapo Kenya pia nasikia Gormahia wamenyanyua ndoo huku pia nikipata ujumbe mfupi wa maandishi kutoka kwa rafiki yangu kuwa Ronaldo hajafunga wiki hii. Mbeya City pia niliwaona wakiumizwa na ndugu zao huku Jerry Murro na jeshi lake wakifanya yao pale taifa ndio kabla ya Simba kufata nyao zao kwenye uwanja huohuo. Kwa haya yote ‘Al-hamdulillah’ ndio neno jepesi sana katika kinywa changu.
Leo hii nimejaaliwa kuandika japo kwa uchache juu ya timu fulani ambayo imekusanya alama 9 katika viwanja 3 ugenini ambavyo vinatumiwa na vigogo wa EPL. Kutokana na hili itakuwa vyema tukiwa wote hadi mwisho wa makala hii tukiitazama West Ham United maarufu kama wagonga nyundo au ‘The hammers’
West Ham ilikuwa ni miongoni mwa timu 3 zilizoteuliwa na UEFA kushiriki michuano ya Europa League kutokana na kucheza ‘Fair play’ kwa msimu wa 2014. Timu zingine 2 zilitoka Uholanzi na Ireland. Japokuwa walitolewa kwenye hatua ya mwanzo kabisa ila halikuwa jambo rahisi kushiriki michuano hii kwani walimaliza nafasi ya 12 kwenye msimamo wa ligi. Kwa sasa wana Meneja mpya ila naamini timu hii ilijengwa vyema na Sam Allardyce ‘BIG SAM’ kwani 2014 walianza vyema licha ya kuharibu baadae. Allardyce aliitengeneza vyema timu hii ili auage vizuri uwanja wa Upton Park na alifanikiwa kwa hili.
Msimu huu wagonga nyundo hawa wameanza upya kwani wapo kwenye Dimba jipya na Kocha mpya pia. Meneja Slaven Bilic ni mzaliwa wa Yugoslavia japokuwa ni raia wa Croatia na ni Mlinzi wa zamani wa West Ham na Everton. Kwa sasa Bilic anainoa timu hii huku akiwa ametokea Uturuki kwenye klabu ya Besktas ambapo mara zote alishika nafasi ya 3 kwenye ligi kuu ya Uturuki. Bilic amekuwa na mwendelezo mzuri wa kuitengeneza West Ham hasa kutokana na uwepo wa wachezaji waliokuwepo msimu uliopita hivyo wametengeneza ‘consistance’ japokuwa huwezi kuwapa dhamana kwa mechi 6 za ligi walizocheza hadi sasa.
Upya wao pia mbali na Uwanja na Meneja, wanae Nahodha mpya pia Mark Noble baada ya Kevin Nolan msimu uliopita. Noble ameendelea kucheza vyema katikati hata kama Song hayupo uwanjani kwani ni mzuri sana kuharibu mashambulizi na kazi hii hajaianza leo kwani utakumbuka West Ham iliwahi kumtaja kiungo huyu kama mchezaji bora wa mwaka mara 2 mfululizo. Upya wa Meneja, Uwanja na Nahodha huenda umeamsha ari kwa timu nzima kwani kila upande unataka mafanikio yakipatikana basi atazamwe wenyewe. Uwepo wa vijana kama Cheikhou Kouyate, Mauro Zarate, Pedro Obiang, Diafra Sakho na Mark Noble umekuwa mwiba sana pale EPL.
Wagonga Nyundo walianza vyema ugenini kwa kuirarua Arsenal 2-0, shukrani kwa magoli ya Mauro Zarate na Kouyate. Kwenye mechi hii Mauro Zarate aliwasumbua sana Arsenal kwani aliharibu mipango ya Wenger sana hasa kutokana na ‘tackles’ alizopiga pamoja na shuti lenye macho ambalo lilimliza Mzee Wenger. Wachezaji kama Dimitri Payer, Kouyate, Diafra Sakho, Aaron Cresswell, Bwana mdogo Reece Oxford na Angelo Ogbonna walionekana kuharibu mipango ya akina Cazorla na Ozil kabisa jambo ambalo liliwapa West Ham wepesi wa kuchukua alama 3 ugenini. Kabla ya mechi hii Arsenal iliipiga West ham mechi 5 mfululizo.
The Hummers walisafiri tena kilometa 289 kwenda Anfield kutoa kipigo kitakatifu cha magoli 3-0 huku nahodha wao akila umeme licha ya kufunga goli la pili. Magoli mengine yalifungwa na Lanzini huku Diafra Sakho akimaliza mwishoni kabisa kabla ya mwamuzi Kevin Friend kupuliza kipenga. Namshukuru Mungu mechi hii niliitazama vizuri na endapo Mark Noble angekuwa makini Liverpool wangelia zaidi. Sakho,Payet, Kouyate, Obiang na Aron Cresswell walicheza vyema huku Ogbonna akiwamaliza kabisa Liverpool. Nadhani unakumbuka licha ya Vijogoo kushinda 2-0 msimu uliopita walitangulia kupigwa 3-1 pale Upton Park.
Kama ilivyo ada Slaven Bilic aliiongoza West Ham kukwea Pipa na kupasua anga takribani kilometa 262 hadi Etihad Stadium kwenda kumsimamisha Manuel Pellagrin ambaye alitengeneza ‘Clean sheat’ katika mechi 5 zilizopita huku akikusanya pointi 15. Unapochukua pointi hata 1 tu pale Etihad Stadium bila shaka wewe ni mwanaume haswa..! Huenda Victor Moses na Sakho wangekuwa makini bila shaka City wangelia zaidi. Payet na Obiang walifanya kazi nzuri sana huku Manuel Lanzini na Winston Reid wakifanya yao. Mark Noble aliwazidi akina Fernandinho huku Tomkins akiharibu mipango kabisa ya Man City.
Kutokana na kukusanya pointi 12 baada ya kushinda michezo 4 ikiwemo 3 ya ugenini ambapo wametoa dozi kwa Liverpool, Arsenal na Man City, West ham wanazidi kuogopwa na vigogo na kudhihirisha kuwa katika msimu huu wa 20 tangu kucheza ligi kuu, The hummers hawana utani na kwa sasa wanahitaji kucheza Europa League kihalali bila upendeleo wowote. Kigogo anayefata ni Chelsea, Spurs na Man united. Naamini wapenzi wengi wa soka wanaisubiri kwa hamu West Ham kwa timu hizi hasa baada ya vipigo kwa vigogo watatu tena katika viwanja vyao.