Kwa mara nyingine tena nyota wa Tanzania Mbwana Samatta ameendelea kung’ara kwenye ligi ya Ubeligiji (Belgium Pro League) baada ya kuifungia timu yake bao moja wakati ikiibuka na ushindi wa magoli 2-1 dhidi ya Zulte-Waregem.
Kwa mara ya kwanza Samatta akicheza kwa dakika zote 90 alifanikiwa kuiweka mbele timu yake mapema dakika ya nane ya mchezo kwa kuzifumania kamba kwa bao la kichwa.
Hilo ni goli la nne kwa Samatta tangu ajiunge na Genk mapema mwaka huu na ni mwendelezo mzuri kwa nahodha huyo wa kikosi cha Stars.
Mara zote Samatta amekuwa akicheza dakika kadhaa za mchezo kwa kupishana na Nikolaos Karelis, mchezo wa Jumamosi usiku Samatta alicheza kwa dakika zote huku mshambulizi mwenzake akisubiri kwenye benchi.
Kama ulipitwa na mechi ya Zulte-Waregem vs Genk, shuhudia kipande cha magoli yote yaliyofungwa kwenye mchezo huo.