Vipigo vitatu vilivyozikumba klabu za Arsenal, Manchester United na Manchester City katika raundi ya kwanza ya makundi ya michuano ya klabu bingwa ulaya, inaleta taswira ya namna timu za England zinavyopoteza uongozi katika hilo la mpira.
Kabla ya kuanza kwa msimu wa ligi kuu nchini England msimu huu, mkurugenzi wa vilabu nchini humo alisema kuwa vilabu vyao vinaweza visifanye vizuri katika michuano hiyo kutokana na kile alichokisema hazijajiandaa vizuri.
Hali hii ikiendelea inaweza kuiondoa England katika nafasi tatu za juu klabu bingwa na serie A ya Italia ikachukua nafasi. Vilabu vya England ukijumuisha na Chelsea ambao ni mabingwa watetezi wa ligi ya ndani pamoja na kufika fainali mwaka 2012 na kuchukua kombe mbele ya Bayern Munich, hawako vizuri na sasa wamefungwa na Porto ya Ureno katika mchezo wa pili wa kundi lao.
Kabla ya mwaka 2011 Manchester United walikua wameingia nusu fainali ya klabu bingwa ulaya mara nne mfululizo huku wakitwaa ubingwa mara moja 2008 na kucheza fainali zingine mbili 2009 na 2011. Hivi sasa ikiwa ndio wamerudi tena, hawaoneshi kama wako sawa kupambana kwa ubingwa.
Klabu za Barcelona, Bayern Munich na Real Madrid zimechukua ubingwa katika klabu bingwa mara nne katika fainali tano zilizopita. Kuanzia 2011 hadi msimu uliopita ni Chelsea pekee walitwaa ubingwa mwaka 2012.
Kustaafu kwa kocha Alex Ferguson wa Manchester United 2013 kuliipoteza United chini ya David Moyes kukwama kufuzu kucheza michuano hiyo mwaka jana. Kitu kilichochangia kupoteza nguvu kwa vilabu vya England barani ulaya.
Nini sababu ya kutofanya vizuri kwa vilabu hivi vya ligi hii inayosemwa bora zaidi barani ulaya?
Ugumu na ushindani wa ligi kuu nchini England ni miongoni mwa sababu za kufeli kwa vilabu hivi barani ulaya. Hili linaungwa mkono na kocha wa Manchester United, Louis Van Gaal ambaye anasema kugombana kushinda ubingwa wa ligi kuu nchini England ama kugombana kufuzu kwa ajili ya michuano hiyo ya ulaya ni kugumu kuliko hata ilivyo michuano yenyewe.
Maneno haya ya Van Gaal yanaweza kuthibitisha uhalisia kwa kile kilichowakuta Chelsea msimu wa mwaka 2012 walipotwaa ubingwa wa ulaya lakini wakaangukia pua katika ligi ya nyumbani walipomaliza nafasi ya sita.
Ili timu ifanye vizuri katika klabu bingwa barani ulaya, shurti ilegeze kamba katika ligi ya nyumbani EPL ili kuwapa nafasi wachezaji kupumzika na kujiandaa vizuri zaidi katika klabu bingwa ulaya.
Kauli hizo za Van Gaal zinapingwa vikali na Scudarmore ambaye ni mkurugenzi wa vilabu nchini England, anaesema, “siamini katika hilo, ingekua hivyo, tusingeweza kuingiza timu tatu nusu fainali mwaka 2008″.
Vilabu vya England pamoja na mkataba mnono wa TV msimu huu, havijawekeza sana katika wachezaji bora kama ilivyo kwa vilabu vya Hispania na Ujerumani.
Manchester United tangu imuuze Ronaldo na kumpoteza Tevez ilianza kupotea katika ramani ya soka la ulaya huku ikivineemesha vilabu vya ligi nyingine.
Msimu huu wakiwa ndio wamerejea katika michuano ya ulaya, wamemuuza Angel Di Maria na kuinufaisha PSG ya ufaransa ambako anafanya vizuri.
Chelsea tofauti na misimu kadhaa nyuma walipokua na kikosi bora zaidi cha akina Lampard, Ballack, Makelele na Drogba wamekua timu isiyokua na uhakika wa kufanya vizuri barani ulaya.
Sera ya usajili ya Arsenal pamoja na kupotea kwa Liverpool katika soka ya Ulaya ni sababu nyingine inayozipoteza klabu za England klabu bingwa hivi sasa.
Uimara wa klabu za Real Madrid, Barcelona na Bayern Munich unatokana na uwekezaji wao walioufanya kuimarisha vikosi vyao ndani ya uwanja.
Usajili wa wachezaji wa kiwango cha dunia wa Gareth Bale, James Rodriguez, Luis Suarez na Neymar ni moja ya chachu kubwa ya kufanya vizuri kwa miamba hii ya nchini Hispania, huku pia kukiwa na uwepo wa wachezaji bora zaidi duniani Lionel Messi na Cristiano Ronaldo.
Bayern Munich wako imara kila idara lakini bado wamewaongeza Arturo Vidal na Douglas Costa kuimarisha uwezo wao na ndio sababu wanafanya vizuri barani ulaya.